Na Fatma Gaffus, Dodoma.
Usafiri wa Reli ya Kati umeanza wakati ujenzi katika Daraja la Godegode wilayani Mpwapwa ukiendelea.
Akizungumza na Star Tv, Mkuu wa Kituo wa Kampuni ya Reli Mkoa wa Dodoma Bwana Flavian Nyawale amesema wamechukua hatua hiyo ya kuanza huduma za safari za Treni kutokaDodomakwenda Kigoma kutokana na maeneo ya Gulwe, Godegode na Kidete kuwa korofi kwa sababu ya mvua kubwa zinazoendelea kunyesha mkoaniDodoma.
Bwana Nyawale amesema kuhusu Treni ya kwenda Mwanza bado haijaanza safari zake kwa sababu wanatafuta fedha za kuweza kutoa huduma hiyo.
Amesema huduma ya usafiri itakuwa inatolewa mara mbili kwa wiki kwa siku ya Jumanne na Jumamosi ambapo Treni za mizigo zinaendelea kupita katika daraja la Godegode wakati ujenzi ukiendelea kwa uangalizi mkubwa.
Baadhi ya Abiria waliosafiri na Treni hiyo ya abira iliyoondoka Januari 24 majira ya saa 1.15 usiku wameishukuru Kampuni ya Reli TRL kwa kuanza kuwapatia huduma hiyo muhimu ambayo waliikosa kwa muda mrefu sasa.
Wamesema walisitisha safari zao kwa kushindwa kumudu gharama za mabasi hasa katika kipindi cha kumaliza likizo kwa wafanyakazi na wanafunzi.
Wameitaka Kampuni ya Reli TRL kushughulikia kero zote ambazo zinajitokeza katika zoezi zima la kurudisha fedha kwa abiria pindi itakapotokea tena hali hiyo ya kukosa huduma za usafiri katika msimu wa mvua ambapo maeneo ya Gulwe, Godegode na Kidete yanakuwa yakisumbua kipindi hicho.
Takribani siku 36 huduma za usafiri katika Kampuni hiyo ilisitisha huduma zake kutokana na kuharibika kwa daraja la Godegode hali iliyosababisha Kampuni hiyo kuwasafirisha abiria wake kwa njia ya barabra kwa kutumia mabasi kutokaDodomakwenda Dar es Salaam.
Mwisho.










