Na Joseph Mpangala,
Dar es Salaam.
Baadhi ya Wataalam wa masuala ya Uchumi nchini wamesema kuchaguliwa kwa Mmarekani Dokta Jim Yong Kim kuwa Rais wa Benki ya Dunia kunaweza kuleta matumaini kwa nchi zinazoendelea katika kuimarisha sekta ya afya.
Dokta Kim ambaye ni Mtaalam wa Afya akiwa na uzoefu wa nchi zinazoendelea ameteuliwa na Bodi ya Benki ya Dunia kushika nafasi hiyo na kuondoa matumaini ya Bara ya Afrika kutoa Rais wa benki hiyo kupitia kwa Ngozi Okonjo Iweala wa Nigeria.
Kuchaguliwa kwa Dokta Kim mwenye asili yaKoreakuwa Rais wa Benki ya Dunia kunaifanya Marekani iendelee kuweka mtu anayetokana na Taifahilokatika taasisi hiyo kwa miaka 68 hivi sasa tangu benki hiyo ilipoanzishwa mwaka 1944.
Dokta Kim ambaye ni Rais wa 12 wa benki hiyo akichukua nafasi ya Rais wa sasa Robert Zoellick anayemaliza muhula wake wa miaka mitano hapo Juni mwaka huu, amepata uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa wajumbe wa Ulaya na Marekani wakiwa ni miongoni mwa nchi wanachama 187 waliopiga kura kupitia Bodi ya Magavana.
Profesa Ibrahim Lipumba ni Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi CUF ambaye ni Mchumi na Mshauri wa muda mrefu katika nchi zilizoendelea, anasema ingawa Bibi Ngozi angewapa matumaini Waafrika lakini kwa Dokta Kim bado kuna matumaini kutokana na sera zake za kuondoa umaskini hasa katika nchi za dunia ya tatu.
Hata hivyo Profesa Humphrey Moshi kutoka Chuo Kikuu chaDar es SalaamUDSM anasema hakuna mabadiliko yoyote yatakayotokea katika uongozi huo mpya kutokana na kwamba tayari taasisi hiyo kubwa ya kifedha duniani imejiwekea sera pamoja na dira ambazo zinahitaji kufanyiwa kazi endelevu.
Dokta Jim Yong Kim tayari ametoa vipaumbele vyake kuwa ni pamoja na kuongeza ajira kwa vijana na kupunguza umaskini katika nchi zinazoendelea ambazo kwa kiasi kikubwa zinaonekana kuwa na umaskini uliopitiliza.
Dokta Kim atakabidhiwa madaraka na mtangulizi wake, Zoellik Juni mwaka huu baada ya kumshinda Bibi Ngozi Okonjo Iweala ambaye amewahi kushika nafasi ya juu katika Benki ya Dunia akiwa miongoni mwa Wakurugenzi wa benki hiyo.
Mwisho
No Comments