Na Violet Kimwaga,
Mwanza.
Taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali zinapaswa kujikita zaidi kwenye maeneo ya vijijini ikiwa ni jitihada za kumkwamua mwanamke katika changamoto mbalimbali zinazokwamisha maendeleo yake ndani ya jamii.
Rai hiyo ilitolewa na mke wa waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bi. Tunu Pinda katika hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na Taasisi isiyo ya kiserikali ya Kangaroo Women Empowerment Association (KWEA) jijini Mwanza.
Bi. Tunu alisema wanawake wanaoishi vijijini wanahitaji msaada zaidi kwani wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ukosefu wa elimu, maradhi na mfumo dume ambazo zinasababisha washindwe kujikwamua kiuchumi hivyo kuishi katika hali duni.
Aidha aliitaka KWEA kuwa chachu ya kuleta maendeleo kwa kuwakwamua kiuchumi wanawake wasiojiweza na kutoa mtazamo chanya kwa jamii kuhusu wanawake ili waweze kupewa kipaumbele katika fursa mbalimbali.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri mkuu Mheshimiwa Mizengo Pinda ambaye amewaasa wanachama wa Taasisi hiyo kuwa na ushirikiano na uadilifu katika kazi ili kuepuka makundi ndani ya Taasisi.
Kangaroo Women Empowerment Association (KWEA) ni Taasisi isiyo ya Kiserikali iliyoanzishwa Januari mwaka huu ikijumuisha wanawake wa kada mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara, madaktari na walimu lengo likiwa ni kumwezesha mwanamke kujikwamua katika changamoto za maisha.
Zaidi ya shilingi milioni ishirini zimetolewakamaahadi katika harambee ndogo iliyofanyika kwenye hafla hiyo kwa lengo la kuijenga zaidi Taasisi hiyo.
No Comments